Monday, July 14, 2008

SWAHILI


Mahmoud Ahmad Mahmoud, HSC

Maelezo binafsi ya Ustadhi Mahmoud Ahmad Mahmoud:
Mahmoud Ahmed Abdulkadir (MAU) nilizaliwa Amu pwani ya Kenya mwaka 1950 nilisoma madrassa Annajah, sikwenda shule za kawaida.

Ni mwalimu wa madrassa, vile vile nahutubu Ijumaa. Nafundisha somo la dini ya Kiislamu katika shule kadhaa za msingi pia naendesha darasa la watu wazima msikitini. Naelewa vyema lugha ya kiswahili na pia kiarabu vizuri na kiengereza kwa kadiri Fulani. Kadhalika naandika mashairir na natumia lahaja ya kiamu. Naandika katika maudhui tofauti tofauti zaidi mambo ya kijamii na vile vile siasa.

Kwa mara ya kwanza nalijitokeza kusoma shairi nililoandika juu ya uhuru wa Kenya baada ya miaka kumi 12/12/1973. kuanzia hapo nilipata umashuhuri nakutangaa kuwa ni mshairi. Mwaka 1974 niliandika “WASIA WA MABANATI” Utendi wenye baiti 140 ambao ulikua ukielezea mikasa iliyompata msichana aliefanya urafiki na mvulana ambae alimtia mimba na baadae akamruka. 1975 – 1979 niliandia tendi tisa kwa jina la kimondo ambazo zilitumika kufanya kampeni wakati wa uchaguzi wa wabunge hapa Lamu. Mimi nilimsaidia Mzamil Omar Mzamil mpinzani wake alikuwa ni Madhubuti na baada ya hapo niliendelea kuandika mashairi lakini mafupi mafupi na sana huwa ni ya watu binafsi kuhusu mambo yao wenyewe k.m harusi, matanga, safari na kadhalika.

Mwaka wa 2000 niliandika tendi mbili, mmoja kwa jina la UZUNDUZI na wa pili MWANGAZA kujaribu kuwahimiza watu wazundukane na watambue haki zao na kuzitetea. Pia niliandika utendi mrefu wa baiti 700 juu ya haki za uraia vile vile niliandika tendi juu ya Ukimwi, Mihadharati na haki za watoto.
2004 niliandika tendi mbili kwa anwani ya ramani ya maisha ya ndoa, mmoja wa mume na wa pili wa mke. Pia nimeandika mashairi mafupi kadha moja ni kuhusu Ahmad Yassin na lingine kuhusu Faluja, IRAQ. Nina nia ya kuandika utendi juu ya haki za wazazi. Babangu pia alikuwa ni mshairir vile vile mamangu. Mtoto wangu wa kwanza ana kipawa cha ushairi lakini haandiki sana.

Mimi nimeoa nina watoto 11, mkubwa na miaka 29 na mdogo ana miaka 8. wasichana ni 7 na wavulana ni wane. Napata mkate wangu wa kila siku kwa uwokaji mikate “BAKERY” kazi ambayo nilirithi kutoka kwa mlezi wangu Ammi yangu, Bwana Abdulghafur Abdulkadir.
Napendelea sana kusoma vitabu mbali mbali zaidi kwa kiarabu. Napenda kuogelea baharini na kusafiri. Kusoma ndio pumbao langu kubwa!! Mwaka jana 2004 nilitunukiwa tuzo ya “THE HEAD OF STATE’S COMMENDATION (HSC- CIVILAN DIVISION).

Sources: ZANZINET SWAHILI POEMS

www.zanzinet.org

No comments: